2013-08-27 15:08:09

Uganda na Italia kuendeleza ushirikiano!


Nchi za Uganda na Italia zimekuwa marafiki wa muda mrefu na zitaendelea kukuza urafiki huo katika jitihada za kuyaimarisha mataifa hayo mawili na kuendeleza maendeleo yao ya kiuchumu na kijamii. Hayo yamesemwa na Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda mwishoni mwa wiki alipokutana na Waziri mdogo wa Mambo ya nje wa Italia, Bwana Lapo Pistelli anayeitembelea Uganda.
Kati ya mambo waliyojadili Rais Yoweri Museveni wa Uganda na mgeni wake Waziri Piselli wa Italia ni mshikamano wa nchi hizo mbili na ustawi wa eneo la Afrika mashariki na hasa hali tete ya Somalia. Bwana Pistelli ameitembelea Uganda kwa lengo la kuboresha uhusiano kati ya Italia na Uganda.
Ni wazi kwamba katika ulimwengu wa utandawazi, mataifa mengi yanatafuta ushirikiano wa karibu ili kuzipa nchi zao kipaumbele cha kwanza katika mambo ya biashara na nchi marafiki. Kwenye mkutano kati ya Waziri Mkuu wa Uganda Bwana Amama Mbabazi na Waziri mdogo wa Mambo ya nje wa Italia Bwana Piselli, ushirikiano kwenye maswala ya kisiasa na kiuchumi yamejadiliwa kwa kina ikiwemo mpango wa mkutano wa kiuchumi kati ya nchi hizi mbili hapo mwezi oktoba 2013.

Mkutano huu unatarajiwa kufanyika nchini Uganda na ambao utayashirikisha makampuni 30 yatakayoiwakilisha Jumuiya ya wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda nchini Italia.








All the contents on this site are copyrighted ©.