Watawa wa Mtakatifu Yosefu Jimbo kuu la Mombasa wanamwimbia Mungu utenzi wa sifa na
shukrani!
Askofu mkuu Boniface Lele wa Jimbo kuu la Mombasa, Kenya, katika Maadhimisho ya Sherehe
ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu
kwa ajili ya Watawa wa Shirika la Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la Mombasa waliokuwa
wanaweka nadhiri zao za daima, wengine wakiadhimisha Jubilee ya Miaka 50 na 25 ya
maisha ya kitawa.
Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Lele amewahimiza watawa
kuongeza upendo, furaha na ukarimu katika huduma wanazozifanya kwa ajili ya Watu wa
Mungu wanaowazunguka, daima wakijifunza kutoka kwa Bikira Maria aliyejitosa bila ya
kujibakiza kwa ajili ya Familia Takatifu. Watawa waendelee kuwa kweli ni mwanga wa
imani kwa kujikatalia mambo ya dunia ili kuambatana na Kristo aliyeteswa, akafa na
kufufuka kutoka katika wafu. Watawa wasimame kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi
kwa njia ya ushuhuda wa maisha na utume wao kwa Kanisa na ulimwengu.
Hii ndiyo
changamoto ambayo Mama Kanisa anaendelea kutoa kwa Watoto wake wakati huu wa Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani. Mapendo na ukweli vinajidhihirisha pale ambapo imani inamwilishwa
katika matendo na hivyo kuwa ni dira inayomwongoza mwamini kumpatia Mwenyezi Mungu
kipaumbele cha kwanza katika maisha na huduma.
Hii ni changamoto ya kupenda
kama Mwenyezi Mungu anavyopenda na kuthamini. Waamini wajitahidi kumwilisha ndani
mwao, fadhila ya imani, matumaini na mapendo. Watambue kwamba, wanatakiwa kuitekeleza
amri ya upendo kwa Mungu na jirani kwa njia ya ushuhuda wa maisha.
Askofu mkuu
Boniface Lele anasema kwamba, maisha ya Sala, Sakramenti na Tafakari ya kina ya Neno
la Mungu yanaweza kumsaidia mwamini kukuza na kuimarisha uhusiano wake na Mwenyezi
Mungu, kiasi hata cha kuweza kujitosa kimasomaso bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu
na jirani. Askofu mkuu Lele anawashukuru watawa kwa majitoleo na moyo wao wa sala
kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu Jimboni Mombasa na sehemu mbali
mbali za dunia wanakotekeleza utume wao.
Shirika la Watawa wa Mtakatifu Yosefu,
Jimbo kuu la Mombasa lilianzishwa kunako mwaka 1941, ili kuwashirikisha waamini furaha
ya ushuhuda wa Injili kwa Kristo na Kanisa lake kwa watu wanaoishi Jimbo kuu la Mombasa
kwa njia ya huduma makini. Katika kipindi cha miaka 73, Watawa hawa wamekuwa wakitoa
huduma katika maisha ya kiroho, kwenye sekta ya elimu, afya na mawasiliano nchini
Kenya, Tanzania, Ulaya na Marekani.
Shirika la Watawa wa Mtakatifu Yosefu
linaongozwa na roho ya Mtakatifu Benedikto, yaani Ora et Labora: Sala na Kazi; daima
wakijitahidi kufuata na kuiga upole, imani na unyenyekevu wa Mtakatifu Yosefu mchumba
wake Bikira Maria na Baba Mlishi wa Mtoto Yesu. Mtakatifu Yosefu ni dira na kielelezo
cha maisha na utume wao ndani ya Kanisa.
Wafuatao wamefunga nadhiri zao za
daima: 1. Sr. Rachel Wakene. 2. Sr. Catherine Furaha, 3. Sr. Josephine Mulunde, 4.
Sr. Phylace Mokaya, 5. Sr. Mary Mutono pamoja na 6. Sr. Gladys Moraa.
Masista
wafuatao wameadhimisha Jubilee ya Miaka 50 ya Maisha ya Kitawa 1. Sr. Hedwiga Mang'oli, 2.
Sr. Blandina Matesha pamoja na 3. Sr. Auxilia Mkasumbuka.
Masista wafuatao
wamemwimbia Mungu utenzi wa sifa kwa Jubilee ya Miaka 25 1. Sr. Jacinta Kivinya, 2.
Sr. Gisela Wanyika, 3. Sr. Agnes Muthoni, 4. Sr. Rose Mbeneka pamoja na 5.
Sr. Bernadette Mwelu.
Imeandaliwa na Sr. Bridgita Samba Mwawasi. Idhaa ya
Kiswahili ya Radio Vatican.