Vitendo vya kigaidi vinapaswa kudhibitiwa, ili kudumisha misingi ya haki, amani, utulivu
na maendeleo!
Ifuatayo ni hotuba ya Mizengo Pinda, Waziri mkuu wa Tanzania, wakati wa kuhitimisha
shughuli za mkutano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 28 Juni 2013.
UTANGULIZI
a) Masuala ya Jumla Mheshimiwa Spika, Tarehe 9 Aprili, 2013 tulianza
Kikao cha Kwanza cha Mkutano wa 11 wa Bunge lako Tukufu. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi
Mungu mwenye wingi wa Rehema kwamba leo tunahitimisha shughuli zote zilizopangwa kwa
amani na salama. Mkutano huu ulikuwa mahsusi kwa ajili ya kuwasilisha, kujadili na
hatimaye kupitisha Bajeti ya Serikali na Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa Wizara,
Mikoa na Taasisi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, Pamoja
na kupitisha Bajeti ya Serikali, katika Mkutano huu Waheshimiwa Wabunge walipata fursa
ya kufanya uchaguzi wa Wajumbe kwenye Taasisi na Vyuo vya Elimu ya Juu. Napenda nitumie
nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Murtaza Ally Mangungu, Mbunge wa Kilwa Kaskazini
kuwa Mjumbe wa Bunge hili katika Chuo Kikuu cha Dodoma; Mheshimiwa Jitu Vrajilal
Soni, Mbunge wa Babati Vijijini kuwa Mjumbe katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo;
Mheshimiwa Dkt. Pindi Hazara Chana, Mbunge wa Viti Maalum, kuwa Mjumbe wa Chuo Kikuu
cha Sayansi na Taknolojia – Mbeya na Mheshimiwa Selemani Said Jafo, Mbunge wa Kisarawe
kuwa Mjumbe wa Jukwaa la Kibunge la Nchi Wanachama Kusini mwa Afrika (SADC – PF).
Aidha, nawapongeza Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge wa Viti Maalum na Mheshimiwa
Mohamed Habib Mnyaa, Mbunge wa Mkanyageni kwa kuchaguliwa kuwa Wawakilishi wetu katika
Baraza la Chuo Kikuu cha Mzumbe. Matarajio yetu ni kwamba, wote waliochaguliwa watatuwakilisha
vyema katika Taasisi hizo muhimu.
Mheshimiwa Spika, Kipekee,
napenda nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Yussuf Salimu Hussein kwa kuchaguliwa
kuwa Mbunge Mpya wa Jimbo la Chambani kupitia Chama cha Wananchi – CUF. Ni dhahiri
kwamba kuchaguliwa kwake ni kutokana na matumaini makubwa waliyonayo Wananchi wa Jimbo
la Chambani na kwamba atawawakilisha vyema ndani na nje ya Bunge katika kusukuma shughuli
za Maendeleo Jimboni mwao.
Vilevile, nitumie nafasi
hii kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Dalali Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga na Mheshimiwa
Aeshi Hilaly, Mbunge wa Sumbawanga Mjini kwa kufanikiwa kurejea tena Bungeni baada
ya kushinda rufaa za kesi zao za uchaguzi katika Majimbo yao.
Mheshimiwa
Spika, Napenda kuchukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uongozi wake makini
ambao umeendelea kuipatia sifa Tanzania katika ngazi za Kanda na Kimataifa. Hali hiyo
imejidhihirisha wazi kwa matukio ya Kimataifa ambayo yamefanyika hapa Nchini. Miongoni
mwa matukio hayo ni Ziara ya Rais Xi Jinping wa China alipotembelea Tanzania
tarehe 24 Machi, 2013, na kuhutubia Bara la Afrika akitumia Jukwaa la Tanzania. Hivi
sasa pia tunajiandaa kumpokea Mheshimiwa Barack Obama, Rais wa Marekani atakayekuwepo
hapa Nchini kuanzia tarehe 1 Julai, 2013. Vilevile, Tanzania itakuwa Mwenyeji wa Mkutano
wa Kimataifa wa Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote wa Mwaka 2013 (Global
2013 Smart Partnership Dialogue) ambao utafanyika kuanzia tarehe 28 Juni, 2013. Matukio
yote haya siyo tu yametokea hivi kwa bahati tu, bali ni muonekano wa Tanzania Nchi
za nje na jinsi ambavyo inaonekana kwa wenzetu tunaoshirikiana nao. Hili ni jambo
la kujivunia!
Mheshimiwa Spika, Sote tunakumbuka
kuwa, wakati tukiendelea na Mkutano huu hapa Bungeni, matukio matatu makubwa ya kusikitisha
yalitokea hapa Nchini. Moja ni tukio la Mlipuko wa Bomu katika Kanisa Katoliki la
Mtakatifu Joseph Mfanyakazi la Olasiti, Arusha lililotokea tarehe 05 Mei, 2013. Pili
ni tukio la vurugu za tarehe 22 Mei, 2013 zilizotokea Mkoani Mtwara baada ya baadhi
ya Wananchi wa Mtwara kutopenda kujengwa kwa Bomba la Kusafirishia Gesi kutoka Mtwara
hadi Dar es Salaam. Tatu ni tukio la mlipuko wa Bomu lililotokea tarehe 15 Juni, 2013
katika Mkutano wa Kampeni za Uchaguzi wa Madiwani katika Kata ya Soweto katika Jiji
la Arusha. Wote tunakumbuka kwamba katika matukio yote haya matatu, Watu wapatao 10
walipoteza maisha na wengine wapatao 155 kupata majeraha, na mali za Raia kuharibiwa
au kupotea kabisa. Kwa masikitiko natoa pole wale wote waliopotelewa na Ndugu, Jamaa
na Marafiki katika matukio hayo. Aidha, nawapa pole Majeruhi wote pamoja na Wananchi
wote waliopoteza mali ikiwemo kuchomewa nyumba na hivyo kuathirika kiuchumi na kisaikolojia.
Mheshimiwa Spika, Uzoefu tunaoupata katika matukio
yote haya ni kwamba hakuna raia mwema anayeipenda Nchi yake anayetamani matukio haya
yatokee ndani ya Nchi yetu. Wananchi wengi wamesikitishwa sana na matukio hayo ambayo
yamepoteza maisha na mali za ndugu zetu. Tunamwomba Mwenyezi Mungu atuepushe na hila
zozote zenye nia mbaya ya kufanya matukio kama hayo kutokea tena kwenye Nchi yetu.
Wito wangu kwa Watanzania wote ni kuwaomba tuwe Wamoja katika kukemea na kulaani matukio
hayo. Ni muhimu tuendelee kuishi kwa Upendo, Amani na mshikamano, kwa maana huo ndio
utamaduni wa Mtanzania.
Mheshimiwa Spika, Wakati
wa Mkutano huu, wapo Waheshimiwa Wabunge wenzetu waliopoteza Ndugu, Jamaa na Marafiki,
ikijumuisha Wapendwa wao, Wazazi, na Watoto. Wote kwa ujumla wao nawapa pole kwa yote
yaliyowafika.
b) Maswali Mheshimiwa Spika, Tangu
tulipoanza Mkutano huu tarehe 9 Aprili, 2013 hadi leo, jumla ya Maswali 489 ya Msingi
pamoja na 1,327 ya Nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali.
Vilevile, Maswali 31 ya Msingi na 27 ya Nyongeza yalijibiwa kwa utaratibu wa Maswali
ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu. Nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote waliouliza
Maswali ya Msingi na ya Nyongeza. Aidha, nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri na Naibu
Mawaziri waliojibu Maswali hayo na kutoa ufafanuzi kwa ufasaha mkubwa.
c) Miswada Mheshimiwa
Spika, Katika Mkutano huu, pia Waheshimiwa Wabunge walipata fursa
ya kujadili, kurekebisha na kupitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali
wa mwaka 2013, [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2013]. Kupitishwa
kwa Muswada huo kutatusaidia kama Taifa kuboresha matumizi ya Sheria husika ikiwemo
Sheria ya Uchaguzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Sheria ya Tume ya Kurekebisha
Sheria, na Sheria ya Utumishi wa Umma. Aidha, Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka
2013 (The Finance Bill 2013) na Muswada wa Sheria wa Kuidhinisha Matumizi ya Fedha
za Serikali wa Mwaka 2013 (Appropriation Bill) yote ilisomwa kwa mara ya Kwanza na
kupitia ngazi zake zote na hivyo kuidhinisha Matumizi ya Serikali ya Mwaka 2013/2014.
Mheshimiwa
Spika, Vilevile, Miswada ifuatayo ilisomwa kwa mara ya Kwanza:
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
2013 [The Constitutional Review (Amendments) Act, 2013];
Muswada
wa Sheria ya Kura ya Maoni wa Mwaka 2013 [The Referendum Act, 2013];
Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Akiba kwa Wafanyakazi wa Mwaka 2013
[GEPF Retirement Benefits Fund Act, 2013];
Muswada
wa Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji, 2013 [The National Irrigation Act, 2013]; na
Muswada wa Sheria ya Takwimu wa Mwaka 2013 [The Statistics Act,
2013].
Mheshimiwa Spika, Napenda kwa dhati kabisa
kuwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa kutumia muda wote wa Mkutano huu kwa ufanisi
mkubwa. Wote mtakumbuka tulianza Mkutano huu kwa changamoto kubwa ya Mabadiliko ya
Mzunguko mpya wa kuwasilisha Bajeti ya Serikali (New Budget Cycle) na pengine kuwepo
hoja na mashaka kuhusu ufanisi wake. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba tumefanya
vizuri sana!! Wote ni mashahidi kwamba Waheshimiwa Wabunge wameweza kujadili kwa kina
na kutoa ushauri wao ambao kwa kiasi kikubwa umezingatiwa na Serikali. Tunajivuna
kwa kupitisha Bajeti ya Serikali kwa kutumia utaratibu mpya na kwa kuzingatia Kanuni
na Taratibu za Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Spika, Nitumie
fursa hii ya kipekee kukupongeza wewe binafsi kwa kubuni na kuridhia utekelezaji wa
utaratibu huu. Aidha, nirudie kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri mliyoifanya
kwa ajili ya maendeleo ya Taifa hili. Lakini kipekee kabisa nimpongeze Waziri wa Fedha
na Wataalam wake kwa kazi nzuri ambayo imeiwezesha Serikali sikivu inayoongozwa na
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukamilisha Bajeti hii baada ya kuzingatia ushauri na maoni
ya Waheshimiwa Wabunge. Ni kweli kwamba haikuwa kazi nyepesi, lakini wote ni mashahidi
kwamba kwa mara ya kwanza tumepata Bajeti nzuri ya Serikali na ya aina yake. Changamoto
iliyoko mbele yetu ni kujipanga vizuri kusimamia utekelezaji wake kwa kukusanya Mapato
yatakayotosheleza mahitaji yaliyoorodheshwa kwenye bajeti hiyo.
II UTARATIBU
MPYA WA MZUNGUKO WA BAJETI (NEW BUDGET CYCLE)
Mheshimiwa Spika, Tumefanikiwa
kukamilisha mchakato wa kuandaa, kuchambua, kujadili na hatimaye kuidhinisha Bajeti
za Mafungu ya Wizara zote, zikiwemo Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala mbalimbali
za Serikali, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka 2013/2014. Hatua hii
itatuwezesha kuanza utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ifikapo tarehe 1 Julai, 2013.
Wakati wa mchakato huu tumejifunza mambo mengi lakini pia tumeona zipo changamoto
mbalimbali ambazo zinahitaji kupatiwa ufumbuzi. Aidha, tumepata maoni na ushauri
mbalimbali kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge na Wadau mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha
Bajeti zijazo ili ziwe bora zaidi na zenye maslahi makubwa kwa Wananchi wetu na Taifa
kwa ujumla. Tutazingatia maoni na ushauri huo tuliopata kutoka kwa Wadau wote.
Mheshimiwa
Spika, Miongoni mwa mafanikio ya utaratibu huu mpya ni pamoja na;
Kwanza: Kuwezesha Serikali kuanza kutekeleza Mpango na Bajeti mapema kuanzia tarehe
1 Julai 2013; na Pili kutoa fursa kwa Serikali kufanya majadiliano mapana na ya kina
na Waheshimiwa Wabunge na kuwezesha kuzingatia maeneo muhimu yanayopaswa kuingizwa
kwenye Mpango na Bajeti katika mwaka mpya wa fedha kabla Bajeti mwaka haijapitishwa.
Mheshimiwa
Spika, Kufuatia mafanikio hayo, kwa utaratibu huu mpya tumeweza
kutenga fedha zaidi katika Sekta za Maji, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Umeme Vijijini
na kutunisha Mifuko ya Mendeleo ya Wanawake na Vijana. Ni faraja kwamba Serikali imefanikiwa
kwa kiasi kikubwa kufanya maboresho zaidi katika Kodi na Tozo mbalimbali ili kupata
fedha za kugharamia mahitaji hayo yaliyojitokeza. Serikali inapongeza Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Bajeti, Kamati zote za Bunge za Kisekta na Wadau wengine kwa mchango wao
wa mawazo wa namna ya kuongeza Mapato ya Serikali ili kukidhi mahitaji hayo ya fedha
yaliyojitokeza wakati wa majadiliano ya Bajeti.
III UFUATILIAJI NA
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA VIPAUMBELE VYA MPANGO WA MAENDELEO NA BAJETI YA 2013/2014
Mheshimiwa
Spika, Katika mwaka ujao wa fedha wa 2013/2014, Serikali imejizatiti
kutekeleza kwa dhati Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Serikali tuliyoipitisha katika
Mkutano huu. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Mheshimiwa Stephen
Wasira (Mb.) pamoja na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. William Augustao Mgimwa (Mb.)
katika hotuba zao na kwenye majumuisho wameeleza kwa kina na kutoa ufafanuzi wa hatua
zitakazochukuliwa na Serikali katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na maelezo hayo mazuri ya Waheshimiwa Mawaziri, napenda kutumia
fursa hii kutoa msisitizo katika maeneo mawili muhimu. Eneo la Kwanza ni kuhusu utekelezaji
wa Vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo na utaratibu mpya wa kusimamia na kufuatilia
Miradi ya Maendeleo chini ya President’s Delivery Bureau. Eneo la Pili ni Kuimarisha
Usimamizi wa Ukusanyaji Mapato na Matumizi ya Serikali.
Utekelezaji wa Vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo na utaratibu mpya wa kusimamia
na kufuatilia Miradi ya Maendeleo chini ya President’s Delivery Bureau.
Mheshimiwa
Spika, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Mwaka 2013/2014 umetayarishwa
kwa mantiki kwamba ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka
Mitano wa mwaka 2011/2012 - 2015/2016. Hivyo, malengo yake yamezingatia utekelezaji
wa vipaumbele vya msingi vya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, ambavyo
ni:
Kuongeza uzalishaji, usafirishaji na usambazaji
wa umeme;
Kuimarisha shughuli za Usafirishaji
na Uchukuzi hususan katika Ukanda wa Kati. Hii inajumuisha kupanua Bandari ya Dar
es Salaam na kuboresha usafiri wa barabara na Reli ya Kati;
Kuongeza uzalishaji na tija katika Sekta ya Kilimo, hususan, katika uzalishaji
wa mazao makuu ya chakula ili kutosheleza mahitaji ya ndani na kupata ziada kwa ajili
ya kuuza nje ya Nchi;
Kuchochea uwekezaji
katika Sekta ya Viwanda, hususan, vile vinavyotumia au kuongeza thamani ya mazao ghafi
yanayopatikana hapa Nchini;
Kuendeleza Rasilimali
Watu na Ujuzi ikiwa ni pamoja na kuimarisha ufundishaji wa Masomo ya Sayansi, Ufundi
Stadi na Teknolojia;
Kuhakikisha upatikanaji
wa huduma bora za jamii; na
Kuboresha huduma
za utalii, biashara na fedha.
Mheshimiwa Spika, Ili
kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mipango yetu ya Maendeleo, imeonekana kuna umuhimu
wa kuimarisha Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini. Katika kuhakikisha kwamba azma hii
inatekelezwa, Serikali imefikia uamuzi wa kuanzisha Mfumo mpya wa ufuatiliaji na tathmini
unaojulikana kama “Matokeo Makubwa Sasa” (Big Results Now) ili kuongeza kasi ya utekelezaji
wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 - 2015/2016). Msingi wa Mfumo
huu ni uwazi katika kupanga shughuli za utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo inayokusudiwa.
Kwa ujumla, Miradi ya Maendeleo na utekelezaji wake inatakiwa isiwe siri kwa Wananchi
au jamii inayolengwa. Hivyo, pamoja na kuainisha shughuli zitakazotekelezwa, Mfumo
huu unabainisha muda, mhusika, rasilimali zinazohitajika, vigezo vya kupimia mafanikio
ya utekelezaji na ni shirikishi.
Mheshimiwa Spika, Vilevile,
Mfumo huu umeanzishwa ili kumwezesha Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla, kusimamia
ipasavyo utekelezaji wa programu na miradi ya kipaumbele ili kuharakisha maendeleo.
Hivyo, kazi za utendaji na uratibu zitakuwa chini ya Ofisi ya Rais, Ikulu, na kusimamiwa
na chombo kitakachojulikana kama “President’s Delivery Bureau-PDB”. Majukumu ya chombo
hicho ni:
Kuchambua kwa utaratibu wa Kimaabara wa Miradi
ya kipaumbele iliyobainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na kuainisha
shughuli zinazopaswa kutekelezwa, muda wa kuanza na kukamilika kwake, malengo yanayotarajiwa,
na kiasi cha fedha kinachohitajika kwa utekelezaji;
Kutayarisha
na kusimamia mikataba ya uwajibikaji wa Mawaziri;
Kutoa
ushauri na kusaidia kutatua vikwazo vya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo; na
Kufanya tathmini ya utekelezaji na kuishauri Serikali juu
ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa na kuwezesha Wizara husika kufikia malengo yaliyowekwa.
Mheshimiwa
Spika, Napenda kubainisha kuwa “Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa”
si Mpango, bali ni Mfumo. Mfumo huu utawezesha kusimamia vizuri zaidi utekelezaji
wa miradi ya maendeleo na majukumu ya Serikali yaliyobainishwa kuwa ni ya kipaumbele
katika kufikia malengo ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Mfumo huu, pamoja na
mambo mengine, unakusudiwa pia kuimarisha Mfumo wa Upimaji wa Wazi wa Utendaji Kazi
Serikalini unaojulikana kama “Open Performance Review and Appraisal System - OPRAS”,
ambao kwa sasa umekuwa hautekelezwi kama ilivyokusudiwa. Kwa kutumia Mfumo huu mpya,
sasa Waheshimiwa Mawaziri watakuwa wanawekeana Mikataba ya Utendaji (Performance Contracts)
na Watendaji walio chini yao. Kwa kuanzia, “President’s Delivery Bureau” itasimamia
utekelezaji wa Awamu ya Kwanza katika maeneo sita (6) yaliyofanyiwa uchambuzi wa kina
wa Kimaabara (Labs) ambao umekamilika hivi karibuni. Maeneo hayo ni Nishati ya Umeme;
Uchukuzi na Usafirishaji; Kilimo; Elimu; Maji; na Ukusanyaji Mapato.
Kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa Mapato na Matumizi ya Serikali
Mheshimiwa
Spika, Pamoja na kuanzishwa kwa utaratibu huu Mpya wa kufuatilia
Miradi, kipengele muhimu kilichozungumziwa katika Mkutano huu ni kuhusu kuimarisha
usimamizi wa ukusanyaji wa Mapato na Matumizi ya Serikali. Michango mingi ya Waheshimiwa
Wabunge iliyotolewa imesisitiza kwamba Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2013/2014 iliyoidhinishwa
na Bunge lako Tukufu inahitaji usimamizi makini na mahiri ili kufikia malengo
tuliyojiwekea. Kwa mantiki hiyo, Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi
wa ukusanyaji wa Mapato na kuhakikisha kwamba kuna uwajibikaji mkubwa wa matumizi
ya Serikali. Miongoni mwa hatua zitakazochukuliwa na Serikali katika mwaka 2013/2014
ili kufikia azma hiyo ni pamoja na zifuatazo:
Kwanza: Kuimarisha uwezo
wa Serikali wa kukusanya Mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi wa misaada kutoka
nje na kutegemea zaidi kodi za biashara za Kimataifa na Kikanda. Hatua hizo zitaambatana
na kusimamia ipasavyo ukusanyanyaji wa mapato yatokanayo na rasilimali muhimu za Taifa
kama vile Madini, Gesi Asilia, Wanyamapori, Misitu, Uvuvi, Ardhi, Vivutio vya Utalii
pamoja na kutumia vizuri fursa za kijiografia zinazotokana na Nchi yetu kupakana na
Nchi Nane jirani zisizokuwa na bahari;
Pili: Sambamba na hatua hiyo, Serikali
itayafanyia kazi mapendekezo ya Kamati yako Maalum uliyoiunda inayoongozwa na Mheshimiwa
Andrew Chenge, Mbunge wa Bariadi Magharibi ambayo umeipa jukumu la kuangalia vyanzo
vipya vya Mapato ya Serikali. Aidha, Serikali itakamilisha utafiti wake unaoendelea
wa kubaini vyanzo vipya na endelevu vya kupata mapato mengi ya ndani. Vilevile, itakamilisha
utafiti wa uchambuzi wa misamaha ya kodi ili kuleta mapendekezo mahsusi ya kupunguza
misamaha isiyo na tija;
Tatu: Serikali itaimarisha usimamizi na udhibiti wa
mifumo yake ya ndani hasa katika eneo la Manunuzi ya Umma. Maafisa Masuuli wa Wizara,
Idara za Serikali zinazojitegemea, Wakala na Taasisi za Umma, Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa zote Nchini wanakumbushwa tena kuzingatia ipasavyo Sheria, Kanuni,
Taratibu na Miongozo ya kifedha na kiuhasibu iliyopo kuhusiana na Matumizi ya Fedha
za Umma. Hii ni pamoja na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima kama vile kugharamia
Semina na Makongamano, Ununuzi wa fulana na Kofia za Sherehe mbalimbali, ununuzi
wa magari ya kifahari, posho mbalimbali, mafuta na matengenezo ya magari
ya Serikali kwa gharama kubwa zisizoendana na ubora uliopatikana. Hatua za Kinidhamu
zitachukuliwa kwa watakaokiuka maelekezo yaliyotolewa;
Nne: Ili kuongeza uwazi
na uwajibikaji wa Serikali kwa Bunge na Wananchi, Serikali imeandaa mfumo imara na
endelevu wa kuhakikisha kuwa Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
na Taarifa za Kamati za Kudumu za Bunge zinazosimamia Fedha za Umma yaani Public Accounts
Committee - PAC na Local Authorities Accounts Committee-LAAC zinapewa umuhimu wa hali
ya juu na kushughulikiwa kikamilifu. Tayari, Katibu Mkuu Kiongozi ameunda Kamati Maalum
ya Makatibu Wakuu yenye wajibu wa kuhakikisha kuwa Taarifa hizo zote zinachambuliwa
vizuri na majibu sahihi yanatolewa kwa wakati. Kamati hii inasaidiwa na Kamati Ndogo
ya Wataalam ambayo pamoja na mambo mengine inafanya uchambuzi wa awali, na pia kupendekeza
kwa Kamati ya Makatibu Wakuu namna bora ya kupunguza uzalishaji wa hoja mpya za ukaguzi;
Tano: Ili
kuimarisha usimamizi wa rasilimali za Umma pamoja na kuongeza ufanisi wa utendaji
kazi Serikalini, Serikali itaendelea kuhimiza uzingatiaji wa Maadili katika Utumishi
wa Umma pamoja na kuteua na kupanga safu ya Viongozi na Watendaji hodari, makini na
wenye sifa stahiki za kitaaluma katika Wizara, Taasisi na Idara za Serikali, Mikoa
na Halmashauri. Watumishi wasio na sifa na wababaishaji hawatapewa nafasi.
IV LISHE
Mheshimiwa
Spika, Mara kwa mara nimekuwa nikilitaarifu Bunge lako Tukufu kuhusu
hali ya Lishe Nchini na athari zake kwa Wananchi hasa kwa Watoto chini ya miaka mitano
na uchumi kwa ujumla. Nimeeleza pia juhudi za Serikali katika kukabiliana na hali
ya Lishe Duni. Nichukue nafasi hii kulitaarifu Bunge kuwa Serikali ya Awamu ya Nne
imeendelea na juhudi zake za kuboresha lishe na kipekee Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amekuwa mstari wa mbele katika
kuongoza juhudi hizo.
Mheshimiwa Spika Kutokana
na juhudi hizo, Tarehe 15 Mei 2013, Mheshimiwa Rais alizindua Mpango wa Kuongeza Virutubisho
kwenye Vyakula kwa kuanzia na mafuta ya kupikia na unga wa ngano. Mpango huo utachangia
kwa kiasi kikubwa sana kupunguza utapiamlo kwa Watoto walio chini ya miaka mitano.
Aidha, tarehe 16 Mei 2013 Mheshimiwa Rais alizindua Kampeni ya Kitaifa ya Kuongeza
Uwajibikaji Katika Lishe Nchini. Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali
wa Serikali, Sekta Binafsi, Washirika wa Maendeleo pamoja na Mashirika Yasiyo
ya Kiserikali. Viongozi hao walipata nafasi ya kutoa na kuthibitisha ahadi zao za
kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha Lishe Nchini.
Mheshimiwa
Spika, Kampeni kama hizo zitaendelea kufanyika katika ngazi za
Mikoa, Wilaya hadi Vijijini ili Elimu ya Lishe Bora ienezwe kwa kasi katika ngazi
zote. Napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuwa mstari
wa mbele katika kuongoza mapambano dhidi ya utapiamlo Nchini. Aidha, nitumie fursa
hii kuwaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha wanaendeleza Kampeni za Elimu ya Lishe katika
Mikoa yao na kusimamia kwa karibu kuhakikisha kwamba kampeni hizo zinaendelezwa hadi
kwenye ngazi za Wilaya na Vijiji.
Mheshimiwa Spika, Vilevile,
nitumie fursa kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, tarehe 8 Juni, 2013 nilihudhuria
Mkutano Maalum ulioandaliwa na Nchi Tajiri na zenye Viwanda vingi Dunani (G8) kuhusu
Lishe Bora na Ukuaji wa Uchumi uliofanyika Jijini London-Uingereza na kuhudhuriwa
na Viongozi kutoka Mataifa mbalimbali. Katika Mkutano huo, nilipata nafasi ya kuelezea
hatua ambazo Serikali imechukua katika kupambana na utapiamlo hapa Nchini. Aidha,
nilieleza bayana malengo tuliyoyaweka ya kupunguza utapiamlo kwa Watoto na akina
Mama kama ilivyobainishwa katika Mkakati wa Lishe wa Kitaifa 2011/2012 - 2015/2016.
Malengo hayo tuliojiwekea ni pamoja na kupunguza udumavu kwa Watoto chini ya miaka
5 kutoka Asilimia 42 hadi Asilimia 27, kupunguza ukosefu wa madini joto kwa Wanawake
wajawazito kutoka Asilimia 48.5 hadi Asilimia 35 na kuongeza unyonyeshaji pekee wa
maziwa ya mama kwa Watoto wadogo bila kuwapa chakula chochote ndani ya miezi sita
kutoka Asilimia 50 hadi Asilimia 60.
Mheshimiwa Spika, Imani
yangu ni kwamba, malengo tuliyojiwekea yatafikiwa iwapo sote tutashirikiana kwa karibu
katika utoaji wa Elimu ya Lishe kwa Wananchi wetu katika ngazi zote. Kwa maana
hiyo, ninawasihi Waheshimiwa Wabunge kuendelea kushirikiana na Serikali kutoa elimu
hiyo katika maeneo yenu ili kutokomeza janga hili la utapiamlo Nchini. Nitumie nafasi
hii kupitia Bunge lako Tukufu kuwashukuru kwa dhati Wadau wote wa Maendeleo kwa kuendelea
kushirikiana na Serikali katika jitihada za kupambana na utapiamlo Nchini.
V SEKTA
YA KILIMO
Hali ya Chakula
Mheshimiwa Spika, Tathmini ya awali ya uzalishaji wa mazao ya chakula katika msimu wa 2012/2013
na upatikanaji wa chakula katika mwaka 2013/2014 inaonesha kuwa uzalishaji katika
mikoa 19 kati ya 25 utakuwa wa kuridhisha na kuna dalili za kuwepo kwa chakula
cha ziada katika Mikoa hiyo. Hivi sasa bei za Wastani za chakula hasa mchele na mahindi
katika masoko mengi Nchini zimeshuka kufuatia uvunaji wa mazao hayo katika maeneo
yanayopata mvua za msimu. Kwa mfano, bei ya mahindi imeshuka kutoka bei ya Wastani
ya Taifa ya Shilingi 774 mwezi Februari 2013 hadi kufikia Shilingi 545 katika mwezi
Mei 2013 na mchele kutoka Shilingi 1,825 hadi 1,413 katika kipindi hicho. Matarajio
ni kwamba bei hizo zitashuka kadri chakula kitakavyoingizwa Sokoni. Ili kujihakikishia
kuwa Nchi inakuwa na chakula cha kutosha, Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula (NFRA)
itaanza ununuzi wa Tani 235,000 za mahindi na Tani 15,000 za mtama Mwezi Julai 2013.
Mheshimiwa Spika, Aidha, Serikali kupitia NFRA
itaendelea na usambazaji wa chakula cha msaada kiasi cha Tani 69,451 kilichoidhinishwa
na kutengwa kwa ajili ya kusambazwa kwa watu wenye upungufu wa chakula katika Mikoa
na Halmashauri zenye upungufu. Nitumie fursa hii kuwaagiza tena Wakuu wa Mikoa na
Wilaya kuwahimiza Wakulima kuhifadhi Chakula cha kutosha kwa mahitaji ya Kaya zao
badala ya kuuza Chakula chote na kusubiri Serikali kuwapelekea Chakula. Aidha, Halmashauri
za Wilaya muda wote ziweke Mikakati madhubuti ya kuzuia ununuzi holela wa Chakula
kutoka mashambani mwa Wakulima.
Uamuzi wa
Serikali kuhusu Muundo utakaotumika kutoa Pembejeo za Ruzuku
Mheshimiwa
Spika, Katika mwaka 2012/2013, Serikali iliendelea kutoa ruzuku
za Pembejeo za Kilimo kwa nia ya kumpunguzia Mkulima gharama za uzalishaji. Ruzuku
ya pembejeo imekuwa ikitolewa kwa kutumia Vocha ambapo Mawakala walichaguliwa na Makampuni
ya pembejeo. Hata hivyo, utaratibu huo uligubikwa na changamoto nyingi zikiwemo
za Vocha kuchelewa kuwafikia Wakulima kutokana na kutowajibika kikamilifu na baadhi
Watendaji wasio waaminifu kuwarubuni Wakulima, na baadhi ya Makampuni kutofikisha
pembejeo kwa wakati. Changamoto hii zimelalamikiwa na Wabunge wengi wakati wanachangia
hotuba ya Wizara ya Kilimo na Chakula na Ushirika.
Ili
kuondokana na changamoto hizo, Serikali imeamua kutumia Mifumo miwili katika utoaji
wa ruzuku ya pembejeo za kilimo katika msimu wa kilimo wa 2013/2014. Mifumo hiyo itahusisha
kuendelea na utaratibu wa Vocha na kuanzisha Mfumo wa mikopo kwa uwiano wa Asilimia
80 Vocha na Asilimia 20 mikopo. Aidha, Serikali imeidhinisha Bajeti ya Shilingi Bilioni
112.46 zikiwemo Shilingi Bilioni 19.972 za ufadhili wa Benki ya Dunia na Shilingi
Bilioni 92.49 za Serikali kwa ajili hiyo.
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2013/2014 Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu upatikanaji
wa Tani 400,000 za mbolea, Tani 40,000 za mbegu bora, Miche Milioni 40 ya Chai na
Kahawa, Tani 2,000 na lita 870,000 za madawa ya pamba na korosho kupitia ruzuku ya
pembejeo. Napenda kuwakumbusha Wakuu wa Mikoa na Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri,
kusimamia kwa karibu upatikanaji na usambazaji wa Mbegu na Mbolea ili kuwasaidia Wakulima
kupata pembejeo hizo mapema. Aidha, nahimiza Sekta Binafsi nayo kuendelea kuingiza
Mbolea, Mbegu bora na Madawa mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza Kilimo Nchini.
Mkakati wa Kuimarisha Mfumo Wa Stakabadhi za Mazao Ghalani Zao
la Korosho
Mheshimiwa Spika, Katika Mkutano huu,
Waheshimiwa Wabunge pia, walizungumzia kwa hisia tofauti Mfumo wa Stakabadhi wa mazao
Ghalani. Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani Maghala umeanzishwa kwa mujibu wa Sheria
ya Stakabadhi Ghalani Na. 10 ya mwaka 2005 kwa lengo la kuwasaidia Wakulima wakiwa
katika vikundi au ushirika kuwa na nguvu ya soko, kupata bei nzuri katika mazao ya
biashara na kuingia katika soko la ushindani ambalo ingekuwa vigumu kutokana na kukosekana
kwa mitaji. Pia, ulianzishwa ili kusaidia kuzuia upotevu wa mazao unaotokana na uhifadhi
dhaifu, na pia kuongezea bidhaa thamani kabla ya kuziuza. Mfumo huu ulianza vizuri
ambapo Wakulima walipata malipo ya kwanza, ya pili na ya tatu (Majaliwa). Hata hivyo,
kwa sasa Mfumo huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazotokana na upotoshaji
unaofanywa na walanguzi na madalali wanaojinufaisha na ununuzi wa mazao kutoka kwa
wakulima kwa kutumia mfumo usio rasmi. Vilevile, wapo Watendaji wasio waaminifu wa
Vyama vya Ushirika, wasimamizi wa maghala na Taasisi za fedha wamechangia kudhoofisha
mfumo huo.
Mheshimiwa Spika, Upo ukweli kwamba,
mafanikio mengi yamepatikana baada ya kuanzishwa kwa Mfumo huo. Kwa mfano, kumekuwepo
na ongezeko la uzalishaji wa Zao la Korosho ikilinganishwa na miaka mitano kabla ya
kuanzishwa kwa Mfumo huu kutoka Tani 71.918 katika msimu wa 2001/2002 hadi kufikia
Tani 158,439 katika msimu wa 2011/2012.
Aidha, bei ya Korosho iliongezeka
kutoka Shilingi 360 kwa kilo katika msimu wa 2003/2004 hadi kufikia Wastani wa Shilingi
1,500 katika msimu wa 2010/2011.
Mheshimiwa Spika, Mfumo
huu pia umesaidia Wakulima kuuza mazao yao kwa kutumia Mizani zinazokaguliwa na Wataalamu
na kupatiwa bei Dira kwa kilo, tofauti na vipimo visivyo rasmi vinavyotumika nje ya
Mfumo wa Stakabadhi Ghalani. Wakulima katika maeneo yanayozalisha Korosho wanafahamu
sana vipimo batili vinavyojulikana kama “Kangomba” ambapo licha ya kipimo hiki kutofautiana
kutoka eneo moja hadi jingine; kwa kutumia “Kangomba” Wakulima wanalipwa bei Dira
ya ujazo mkubwa kuliko ujazo wa Kilo moja ya kawaida au kulipwa kidogo kulingana na
bei Dira iliyopo. Aidha, matumizi ya “Kangomba” yanamkosesha Mkulima malipo ya majaliwa
na hata pembejeo za mkopo, maana kipimo hiki hakipo katika Mfumo wa kukopesha Wakulima
Pembejeo.
Mheshimiwa Spika, Chini ya Mfumo huu,
Mikopo kutoka Mabenki kupitia kwa Vyama vya Ushirika vya Msingi imeongezeka kutoka
Shilingi Bilioni 36.2 katika msimu wa 2007/2008 hadi kufikia Shilingi Bilioni
134.6 katika msimu wa 2011/2012. Kwa upande wa mapato, kumekuwepo na ongezeko la
Mapato yatokanayo na Korosho Ghafi kutoka Tani 99,106 msimu wa 2007/2008 hadi Tani
158,439 msimu wa 2011/2012. Thamani ya mauzo imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 43.1
msimu wa 2007/2008 hadi Shilingi Bilioni 236.1 msimu wa 2011/2012.
Aidha, Mapato yatokanayo na ushuru kwa kuuza nje ya Nchi yameongezeka kwa
kiasi kikubwa kutoka Shilingi Bilioni 6.4 msimu wa 2007/2008 hadi kufikia Shilingi
Bilioni 35.4 katika msimu wa 2011/2012. Vilevile, Mfumo huu umewezesha upatikanaji
wa takwimu sahihi za kiasi cha Korosho kilichozalishwa, kilichouzwa nje ya Nchi na
kilichobanguliwa hapa Nchini.
Mheshimiwa Spika, Kutokana
na mifano hiyo michache ya mafanikio, napenda kuchukua fursa hii kuwahakikishia Waheshimiwa
Wabunge, Wakulima na Wananchi kwa ujumla kuwa, Serikali ina imani na Mfumo huu wa
Stakabadhi za Mazao Ghalani, na hivyo hautaondolewa kwa sasa bali Serikali inajipanga
vizuri kuondoa vikwazo vilivyofanya Mfumo huu kufanya vibaya. Tutaimarisha usimamizi
ili kutoa matokeo yaliyolengwa. Aidha, uamuzi huu wa Serikali unatokana na ukweli
kuwa Mfumo huu upo kwa mujibu wa Sheria ya Stakabadhi za Mazao Gahalani Na. 10 ya
mwaka 2005.
Mheshimiwa Spika, Vilevile, katika
mwaka huu Serikali kwa kushirikiana na Wamiliki na wenye Viwanda vya Kubangulia Korosho,
itafanya uchambuzi wa kina wa matatizo yanayokabili Viwanda hivi ili viweze kutumika
kwa ajili ya kununua Korosho kutoka kwa Wakulima na kuzibangua. Lengo letu ni kuhakikisha
kuwa Korosho zote zinazozalishwa hapa Nchini zinabanguliwa na kuongezwa thamani ili
Mkulima aweze kupata bei nzuri zaidi.
Mikakati
ya Kuimarisha zao la Pamba.
Mheshimiwa Spika, Katika
miaka ya hivi karibuni, uzalishaji wa zao la Pamba umekuwa ukidhoofika kutokana na
kukumbwa na changamoto nyingi. Kwa mfano, katika msimu wa Kilimo wa 2012/2013 Kanda
ya Magharibi ililenga kulima wa Hekta 660,000 lakini iliweza kulima Hekta 420,000
tu sawa na Asilimia 64 ya lengo. Upungufu huu ni sawa na Asilimia 26 ikilinganishwa
na Hekta 568,000 zilizolimwa msimu wa kilimo 2011/2012.
Mheshimiwa
Spika,
Changamoto zinazokabili zao la Pamba kwa sasa ni pamoja
na matumizi madogo ya pembejeo zikiwemo mbegu bora na viuatilifu visivyokidhi mahitaji;
na wakati mwingine vimekuwa hafifu kutokana na mfumo wa kusambaza pembejeo hizi kutosimamiwa
vyema. Aidha, katika Mfumo wa Kilimo cha Pamba cha Mkataba ambao unapaswa kumwezesha
Mkulima kupata pembejeo kwa njia ya mkopo nao umeingia dosari nyingi kutokana
na kuwepo kwa baadhi ya Viongozi na Wafanyabiashara katika maeneo yanayolimwa pamba
kuwashawishi Wakulima kuukataa Mfumo huo. Imebainika kwamba baadhi ya Viongozi hao
wana maslahi binafsi katika biashara ya pamba.
Aidha,
Taasisi zinazotakiwa kusimamia Zao la Pamba zimekuwa hazifanyi kazi zake ipasavyo,
Wakulima kukosa imani na Mfuko wa Kuendeleza Zao la Pamba na Vikundi vya Wakulima
kutoandikishwa kisheria hivyo kukosa dhamana ya kufidia wanunuzi endapo watashindwa
kurejesha fedha za pembejeo na mikopo mingine waliyopewa ndani ya Mkataba.
Mheshimiwa
Spika, Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba tayari, Mikutano
ya Wadau inayoshirikisha Wakuu wa Mikoa, Wenyeviti wa Halmashauri, Maafisa Kilimo,
Waheshimiwa Wabunge, Wafanyabiashara wa Pamba, Wakulima, Viongozi wa Bodi ya Pamba,
Wawakilishi wa Wafadhili na Serikali imeshaanza katika Mikoa ya Mara, Simiyu, Geita
na Mwanza. Lengo la mikutano hiyo ni kujadili Changamoto zinazokabili Sekta hii ya
Pamba na kuweka mikakati ya kukabiliana nayo. Mikutano kama hiyo inatarajiwa kuendelea
katika Mikoa yote inayozalisha Zao la Pamba.
Hatimaye tarehe 4 -
5 Julai, 2013 utafanyika Mkutano wa Wadau wote wa Pamba ambao utajadili changamoto
na utatuzi wake.
VI VYAMA VYA USHIRIKA
Mikakati ya kuimarisha
Ushirika Nchini
Mheshimiwa Spika, Vyama vya Ushirika
vimeendelea kutoa mchango mkubwa katika Maendeleo ya Wananchi katika Sekta mbalimbali
za uchumi. Aidha, idadi ya Vyama imeendelea kuongezeka kutoka 5,424 mwezi Machi 2012
hadi 5,559 mwezi Machi 2013. Idadi ya wanachama nayo imeongezeka kutoka 917,889 hadi
1,153,248 katika kipindi hicho. Hisa, Akiba na Amana za Wanachama zimeongezeka
pia kutoka Shilingi Bilioni 236.8 hadi Shilingi Bilioni 463.5
katika kipindi hicho. Kadhalika mikopo iliyotolewa na SACCOS kwa Wanachama wake
imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 703.3 hadi Shilingi Bilioni 893.7.
Mheshimiwa
Spika, Pamoja na mafanikio hayo, pamekuwepo na changamoto mbalimbali
zinazokwamisha kasi ya ukuaji wa Ushirika Nchini. Baadhi ya changamoto hizo zimeongelewa
sana ndani ya Bunge na Waheshimiwa Wabunge. Changamoto hizo ni pamoja na kuwepo kwa
Viongozi wanaodhoofisha ushirika kwa kukosa ubunifu na kutowajibika katika kutekeleza
majukumu yao. Kwa mfano, katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2010 hadi Juni
2012, jumla ya Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS) 1,844 na Vyama vya
Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS) 2,544 vilikaguliwa. Matokeo ya ukaguzi huo yalionesha
kukithiri kwa wizi, ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka kwenye Vyama vya Ushirika.
Vitendo hivyo vimefanywa na Viongozi na Watendaji wa Vyama husika. Kutokana na tabia
hiyo, baadhi ya vyama vimeingia katika migogoro na madeni makubwa na hivyo kusababisha
hasara za mara kwa mara na kuchangia kukatisha tamaa Wanachama kuhusu Ushirika.
Mheshimiwa
Spika, Katika kukabiliana na changamoto hizi, hatua kadhaa zimechukuliwa
ambapo Viongozi wabadhirifu wameondolewa katika Vyama vya Ushirika vya CORECU (Pwani),
CETCU (Singida), MLIMANI SACCOS (Dar es Salaam), AIRPORT TAX DRIVERS (Dar es Salaam),
TUCOPROCOS (Turiani), UWAWAKUDA (Mvomero), MOCEMA (Morogoro), TINGATINGA ARTS SOCIETY
LTD (Dar es Salaam), LUICHE SACCOS (Dar es Salaam), WAZALENDO SACCOS (Moshi) na WETCU
(Tabora).
Pamoja na hatua ya kuwaengua katika nafasi
za uongozi, hatua za kuwatoza fidia (SURCHARGE) pia zimechukuliwa ili kurejesha fedha
zilizofujwa. Aidha, utaratibu wa kuwachukulia hatua zaidi za kijinai unaandaliwa.
Ili kuimarisha ukaguzi na usimamizi, Serikali itaunda timu imara ya ukaguzi zikihusisha
Wakaguzi kutoka Halmashauri za Wilaya mbalimbali zitakazoweza kufanya kazi kwa pamoja.
Hatua hii itasaidia kupunguza uhaba wa Wakaguzi waliopo sasa na kuongeza kasi ya kufanya
ukaguzi.
Mheshimiwa Spika, Vilevile, pamoja
na mipango kadhaa ya kukabiliana na changamoto zilizojitokeza, Serikali itaendelea
kuchambua na kutathmini mienendo ya kiuchumi ya Vyama vya Ushirika katika ngazi zote
za Vyama vya Ushirika vya Msingi, Vyama Vikuu, Vyama vya kilele na Shirikisho la
Vyama vya Ushirika ili kubaini hali halisi ya Vyama hivyo na uwezo wake. Hatua hii
itaiwezesha Serikali kutoa ushauri kuhusiana na wimbi la utitiri wa Vyama vidogo vidogo
ambavyo kimsingi havina tija.
Mheshimiwa Spika, Napenda
kusisitiza kuwa, Serikali imebaini kuwa matatizo ya Ushirika yanasababishwa na udhaifu
katika usimamizi na kwamba tatizo hili pia limetokana na utaratibu wa Maafisa
wa Serikali kuwajibika katika Mamlaka mbili tofauti yaani Serikali Kuu na TAMISEMI.
Hivyo, Serikali imefanya marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Ushirika ya mwaka 2003
ili kuongeza mbinu za usimamizi. Pia, Serikali itaanzisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika
na kuweka Mamlaka ya Usimamizi wa Vyama vya Ushirika katika ngazi zote, chini
ya Mamlaka ya Tume.
Muswada huo tayari umesomwa kwa mara ya Kwanza
na unatarajiwa kusomwa kwa mara ya Pili katika Bunge la Mwezi Agosti 2013.
VICOBA
Mheshimiwa Spika, Pamoja
na changamoto za Ushirika, yapo maeneo ambayo tumeweza kufanya vizuri na ninaamini
tukiyapatia msukumo tunaweza kubadili maisha ya Wananchi wetu. Moja ya maeneo hayo
ni katika VICOBA. Mfumo wa VICOBA umeendelea kushamiri na kuenea katika maeneo mbalimbali
Nchini. Wananchi wengi hasa wa kipato cha chini wamejiunga na kunufaika na Mfumo huu.
Inakadiriwa kuwa takriba Asilimia 35 ya Wananchi wanatumia huduma za fedha zisizo
rasmi ambazo ni pamoja na VICOBA. Aidha, taarifa zilizopo zinaonesha kuwa tangu mwaka
2000 hadi sasa, inakadiriwa kuwa VICOBA vimefikisha Mtaji wa zaidi ya Shilingi Bilioni
300. Kwa sasa kasi ya kukua kwa mtaji imekuwa kubwa ambapo mtaji unakua kwa Shilingi
Bilioni 100 kwa mwaka, tofauti na vilipoanza. Serikali inatambua hali hiyo na imejipanga
vizuri kusaidia uendelezaji wa VICOBA nchini kwani mfumo huu ni rahisi na unasaidia
sana upatikanaji wa huduma za fedha kwa watu wakipato cha chini hasa Wananchi wanaoishi
Vijijini.
Mheshimiwa Spika, Ili kutoa msukumo katika
suala zima la kuendeleza VICOBA, tayari Serikali imeshafanya mambo yafuatayo ili kuimarisha
VICOBA Nchini:
Kwanza: Serikali imeshaanzisha Dawati maalum la kushughulikia
VICOBA katika Baraza la Uwezeshaji wa Wananchi kwa kumteua Ofisa maalum wa kusimamia
VICOBA;
Pili: Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imemteua Mtaalam
Mwelekezi (Consultancy), Kampuni ya DAI Johannesburg ya Afika ya Kusini ili kufanya
Utafiti (Study) na kuishauri Serikali namna bora ya kuendeleza VICOBA Nchini; na
Tatu: Wizara
ya Fedha inaanzisha Idara ya Huduma Ndogondogo za Fedha (Microfinance Deptartiment)
ili kusimamia maendeleo ya Sekta ya Fedha na Idara hiyo ndio itakuwa Mlezi wa VICOBA.
Mheshimiwa
Spika, Pamoja na hatua hizo nilizozitaja, Serikali itaendelea kushirikiana
na Wadau mbalimbali ili kuhakikisha huduma za fedha zinapatikana hadi Vijijini. Kila
Halmashauri, ihakikishe kwamba, mafunzo yanatolewa kwa Vikundi vya VICOBA na vile
vinavyoendeshwa vizuri vipewe fursa zaidi ya kujiendeleza. Kipekee kabisa napenda
kuchukua nafasi hii kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Devota Mkuwa Likokola (Mb.) kwa
jitihada zake kubwa za kuendeleza VICOBA Nchini. Serikali itaendelea kuunga mkono
juhudi hizo pamoja na Wadau wote wa VICOBA hapa Nchini.
VII AJIRA KWA
VIJANA
Mheshimiwa Spika, Katika Mkutano huu, suala la ajira
ya Vijana limezungumzwa sana. Tatizo la ajira bado ni changamoto kubwa inayowakabili
Vijana Nchini. Kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Vijana (2007) umri wa Kijana ni
miaka 15 - 35 Kutokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, idadi ya Vijana Nchini
ni 16,195,370 (Bara na Zanzibar). Idadi hii ni sawa na Asilimia 35.1 ya Watanzania
wote. Vijana walioajiriwa katika Sekta ya Umma ni 188,087, waliajiriwa katika Sekta
Binafsi ni 1,028,634 na waliojiajiri wenyewe ni 1,102,742. Kwa mantiki hii Vijana
waliobaki wapatao 13,200,000 wengi wao wanajishughulisha na Kilimo. Hata hivyo, kwa
vile Vijana hao waliopo kwenye kilimo hawafanyi kilimo cha kisasa na chenye tija,
wengi wao hawafanyi Kilimo cha kibiashara hivyo wako chini ya kiwango cha ajira kamili
kinachofahamika Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, Kwa
kutambua umuhimu wa Vijana katika Nchi yetu, ndiyo maana Mfuko wa Maendeleo ya Vijana
umeboreshwa kwa kuongezewa fedha Bilioni Tatu (3) ili kukuza uwezo wa kutoa
Mikopo yenye masharti nafuu kwa Vijana na kuwajengea uwezo wa kuanzisha shughuli
za uzalishaji mali au kuziimarisha zile wanazoziendesha. Kiasi hicho cha fedha ni
nyongeza kwa Bajeti iliyotengwa kwa mwaka huu wa fedha. Fedha hizi zitatumika kwa
Vikundi vya Vijana waliomaliza Vyuo na Vijana wengine watakaokuwa tayari kuanzisha
miradi mizuri inayokopesheka. Fedha hizi zitaendelea kutolewa kupitia SACCOS za Vijana
za Wilaya. Mwongozo mpya wa Matumizi ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana umesambazwa kwa
Halmashauri zote 151 Tanzania Bara na kwamba Miradi ya Vijana sasa itahakikiwa kwenye
ngazi ya Halmashauri, Mkoa na Wizara kabla ya mkopo kutolewa. Natoa wito kwa Vijana
hasa wakiwa katika Ushirika kuchangamkia fursa hii ili waweze kujiajiri. Nawasihi
wafike katika Mamlaka husika kupata maelezo na kuwasilisha michanganuo ya kazi zao
ili waweze kusaidiwa.
VIII MIGOGORO YA ARDHI
Mgogoro
wa Ardhi kwenye eneo la Pori Tengefu Loliondo
Mheshimiwa Spika, Tarehe 19 Machi 2013, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, ilitoa
Taarifa kwa Umma kuhusu kusudio la kupunguza ukubwa wa eneo la Pori Tengefu la
Loliondo, kutoka Kilomita za Mraba 4,000 hadi 1,500. Lengo la Serikali lilikuwa ni
kulinda mazalia ya Wanyamapori, Mapito na Vyanzo vya Maji kwa ajili ya ustawi wa Hifadhi
katika eneo la Kilometa za Mraba 1,500 lililopendekezwa. Vilevile, ni kuhakikisha
kuwa usimamizi endelevu wa Hifadhi za Serengeti, Ngorongoro na Pori Tengefu la Loliondo
kwa ajili ya Kizazi cha sasa na kijacho.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na taarifa hiyo, Wananchi wanaoishi katika Vijiji vilivyomo ndani
ya eneo la Pori Tengefu Loliondo na ambao wamekuwa wakiishi katika eneo hilo kwa muda
mrefu, hususan katika eneo la Kilomita za Mraba 1,500 ambazo Serikali iliamua ziendelee
kubaki na hadhi ya Pori Tengefu, wamepata hofu ya kuhamishwa na hivyo walituma Wawakilishi
mbalimbali kufika Dodoma na Arusha kuniona ili kupata ufafanuzi wa Tamko hilo.
Mheshimiwa
Spika, Kimsingi, Sheria ya Uhifadhi wa aina mbalimbali za Wanyama
(Fauna Conservation Ordinance) Sura ya 302 ya Mwaka 1951 ndiyo iliyoanzisha Mapori
ya Akiba na Mapori Tengefu Nchini. Sheria hii ilianzisha Mapori Tengefu 49 Nchini
kwa Tangazo la Serikali.
Mwaka 1974, Sheria ya Hifadhi
ya Wanyamapori ilianzishwa na kufuta Sheria ya awali ya Fauna Conservation Sura ya
302. Chini ya Sheria hizo mbili, masuala ya malisho na makazi hayakukatazwa katika
maeneo ya Mapori Tengefu ikiwemo Pori Tengefu la Loliondo. Sheria hiyo ya Hifadhi
ya Wanyamapori iliendelea kutumika hadi mwaka 2009 ambapo Sheria mpya ya Uhifadhi
wa Wanyamapori (The Wildlife Conservation Act) Namba 5 ya Mwaka 2009 ilipoanzishwa
na kufuta ile ya awali ya mwaka 1974.
Chini ya Sheria
hii mpya ya Mwaka 2009, masuala ya malisho na makazi katika maeneo ya Mapori Tengefu
yamezuiliwa, mpaka kwa kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori. Kutokana na masharti
hayo ya Kisheria, Vijiji ambavyo awali vilianzishwa katika maeneo ya Mapori Tengefu
vimejikuta katika hali ya kuvunja Sheria hiyo ya Mwaka 2009.
Mheshimiwa
Spika, Ndani ya eneo la Loliondo ambalo Serikali inapendekeza liendelee
kubaki na hadhi ya Pori Tengefu la Kilomita za Mraba 1,500 kutokana na umuhimu wake
kiuhifadhi, kuna Vijiji sita (6) vilivyosajiliwa na Serikali. Kutokana na Tamko lililotolewa,
ni dhahiri kuwa Wananchi waliopo katika Vijiji hivyo watatakiwa kuhama katika maeneo
hayo. Hata hivyo, changamoto iliyopo ni kwamba, Vijiji vyote hivi vimeanzishwa na
Serikali na kupewa hadhi ya kuwa Vijiji, ingawa kwa mujibu wa Sheria ilibidi ardhi
hiyo iondolewe kwenye hadhi ya Pori Tengefu kwanza kabla ya kuanzisha Vijiji hivyo.
Vijiji hivi vimekuwa ni makazi ya Watu na vina miundombinu ya kudumu ya kutoa huduma
kwa Jamii.
Mheshimiwa Spika, Wananchi waishio katika
Vijiji ndani ya Pori Tengefu la Loliondo wana hofu ya kukosa eneo la malisho ya mifugo
na eneo la kuishi baada ya kuishi hapo kwa miaka mingi kabla na tangu kuanzishwa rasmi
kwa Vijiji hivyo. Hofu ya kuharibiwa kwa hifadhi hiyo ipo pia kwa upande wa Serikali,
na ndio maana Wizara ya Maliasili na Utalii imekuja na Mpango huu wa kuondoa eneo
la Kilomita za Mraba 2,500 ili liwe nje ya Hifadhi na kusimamiwa na Wananchi wenyewe
kwa kuzingatia Mpango endelevu wa Matumizi Bora ya Ardhi.
Mheshimiwa Spika, Napenda kuchukua nafasi hii kulijulisha Bunge lako Tukufu na Wananchi wa
Loliondo kuwa, pamoja na kwamba Tamko la Serikali lilitolewa kwa nia njema ya kuendeleza
uhifadhi endelevu, kumejitokeza malalamiko mengi dhidi ya Tamko hilo. Serikali imepokea
malalamiko hayo kutoka kwa Wadau na Makundi mbalimbali ya Wananchi kutoka Loliondo
wakiwemo Viongozi wa Wilaya, Halmashauri, Wazee wa Kimila, Akina Mama na Vijana.
Mheshimiwa
Spika, Uko ukweli kwamba, suala hili limeleta changamoto kubwa ambayo
inahitaji tafakuri kubwa. Kwa kuzingatia changamoto hizo Serikali kwa sasa inafanya
mambo yafuatayo:
Kupitia upya Tamko lililotolewa na Wizara
ya Maliasili na Utalii kwa kuzingatia Sheria zilizopo za Wanyamapori pamoja na zile
za Ardhi;
Kubaini miundombinu iliyopo katika eneo linalopendekezwa
kubaki na hadhi ya Pori Tengefu;
Kuangalia changamoto
zilizojitokeza kwa pande zote mbili (Wananchi na Serikali) kuhusu eneo hilo la Kilomita
za Mraba 1,500 kuendelea kubaki na hadhi ya Pori Tengefu; na
Kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kuendeleza uhifadhi katika Pori la Loliondo
kwa kuwashirikisha Wananchi.
Mheshimiwa Spika, Wakati
Serikali ikiendelea na hatua hizo, ninawaomba Wananchi waliomo ndani ya Pori hilo
la eneo la Loliondo waendelee kuvuta subira wakati Serikali ikiendelea kutafuta suluhu
ya kudumu ya suala hili. Aidha, nimekwisha toa maelekezo ya awali kuhusu namna ya
kushughulikia ufafanunuzi wa suala hili kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ili kutoa ufafanuzi
stahiki kwa Wananchi wanaoishi ndani ya Pori Tengefu Loliondo. Nawaomba Wananchi
wa Loliondo waelewe nia hii njema ya Serikali ya kuwaondolea wasiwasi uliopo.
Mwisho niwaombe Viongozi wa kisiasa wakiwemo, Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo
la Ngorongoro, Waheshimiwa Madiwani wa Kata za Loliondo na Sale na Viongozi wa Serikali
wa Wilaya ya Ngorongoro na Mkoa wa Arusha watusaidie kusimamia suala hili ili lishughulikiwe
kwa manufaa ya Taifa na Wananchi wa eneo hilo kwa ujumla. Aidha, tuendelee kuhifadhi
mazingira ya eneo hili ambalo limepata sifa kubwa Duniani kutokana na kuwa na vyanzo
vya maji na mapito ya Wanyama Pori wahamao katika Mfumo wa Ekolojia ya Serengeti.
Kwa sasa Dunia inatambua eneo hili kama “Urithi wa Dunia” (World Heritage) na mojawapo
ya Maajabu Saba ya Asili katika Bara la Afrika.
IX MATOKEO
YA UCHAGUZI
Uchaguzi Mdogo
Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imefanikiwa kusimamia Uchaguzi Mdogo wa Ubunge
Jimbo la Chambani, Pemba na Chaguzi Ndogo za Madiwani katika Kata 26 za Halmashauri
mbalimbali Nchini. Vyama vilivyoshiriki katika Chaguzi hizo Ndogo ni CCM, CHADEMA,
ADC na CUF. Matokeo yanaonesha kwamba, Wagombea wa Chama cha Mapinduzi wamefanikiwa
kushinda katika Kata 16 na CHADEMA walipata Kata sita (6) katika Kata 22 ambako uchaguzi
ulifanyika. Chama cha ADC na Chama cha CUF vyote havikupata kura. Kwa upande wa Ubunge
katika Jimbo la Chambani, wote tumeshuhudia kuapishwa kwa Mheshimiwa Yussuf Salim
Hussein kuwa Mbunge Mpya wa Jimbo hilo kwa tiketi ya Chama cha CUF. Nitumie nafasi
hii tena kupongeza Vyama vyote vilivyoshiriki na hasa vile vilivyopata ushindi.
Maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Ngazi ya Vijiji, Mitaa
na Vitongoji Mwezi Oktoba 2014
Mheshimiwa Spika, Tarehe
10 Aprili, 2013 nilitoa tarifa hapa Bungeni kwamba, uchaguzi wa Viongozi katika ngazi
za Vijiji, Mitaa na Vitongoji unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, 2014. Ofisi yangu
inaendelea kuratibu maandalizi ya awali ya Uchaguzi huo ili kuwezesha uchaguzi huo
kufanyika Kidemokrasia zaidi, kwa uhuru na haki. Kwa mujibu wa Kifungu cha 56 (3)
cha Sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura 287 na vifungu vya 4 na 70(c)
vya Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka ya Miji) Sura 288 matoleo ya 2002, jukumu
la msingi la Ofisi yangu ni kuandaa Kanuni za uendeshaji Uchaguzi huo ili kuhakikisha
demokrasia inakuwepo.
Mheshimiwa Spika, Maandalizi
yanayoendelea hivi sasa ni pamoja na kupokea michango na maoni ya awali kutoka kwa
Wadau mbalimbali hususan Vyama vya Siasa kuhusu namna ya kuboresha Kanuni za Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa. Kanuni hizo zinatarajiwa kutangazwa katika Gazeti la Serikali
mwaka 2014. Maoni yanayokusanywa yatachambuliwa na kisha kujadiliwa katika Vikao
vya Wadau vitakavyoitishwa. Aidha, mapendekezo ya Kanuni hizo yatatangazwa kwenye
magazeti ili Wananchi waweze kuzisoma na kutoa maoni yao. Wito wangu ni kuwataka
Viongozi wa Vyama vya Siasa, Vyama Visivyo vya Kiserikali na Wananchi kwa ujumla kujitokeza
kwa wingi katika kutoa maoni ili hatimaye kuwa na Kanuni za Uchaguzi zitakazosaidia
kuwa na Uchaguzi Huru na wa haki.
Mheshimiwa Spika, Maandalizi
mengine yanayofanywa na Ofisi yangu ni kuhakiki Vijiji na kuvisajili. Kabla ya Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa ngazi za Vijiji, Vitongoji na Mitaa wa mwaka 2009 kufanyika,
Vijiji na Mitaa mipya ilianzishwa. Maeneo mapya ya Vijiji yalihakikiwa na kutolewa
hati za usajili kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa. Kwa sasa, Ofisi yangu
imekuwa ikipokea maombi mbalimbali ya kuanzisha Vijiji vipya. Tayari nimetoa maelekezo
kwamba mwisho wa kupokea maombi kwa ajili ya maeneo mapya ya Vijiji ni tarehe 31 Desemba,
2013. Natoa wito kwa Halmashauri zote zinazotaka kuomba Vijiji vipya kuzingatia Sheria,
na tarehe ya mwisho ya kupokea maombi hayo. Aidha, nawaomba kuwashirikisha Wananchi
na Wadau mbalimbali kupitia Vikao vya Ushauri vya Wilaya (DCC) na Mkoa (RCC) ili tuweze
kufanikisha maandalizi ya Chaguzi hizo.
X HIFADHI YA MAZINGIRA
Wiki ya Mazingira Duniani
Mheshimiwa Spika, Tarehe
1 - 6 Juni, 2013 Nchi yetu iliungana na Nchi nyingine Duniani kuadhimisha wiki ya
mazingira Duniani. Maadhimisho hayo yalifanyika Kitaifa katika Wilaya ya Nkasi Mkoani
Rukwa. Ujumbe wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu ni: “Fikiri,
Kula: Hifadhi Mazingira” au kwa Lugha ya Kiingereza “Think - Eat - Save”. Ujumbe huu
unamaanisha kwamba shughuli zote zinazofanyika za uzalishaji mali na utoaji wa huduma
zizingatie kuhifadhi Mazingira badala ya kuwa chanzo cha uharibifu wake.
Mheshimiwa
Spika, Juhudi za kukabiliana na uharibifu wa mazingira zinakabiliwa
na Changamoto mbalimbali. Baadhi ya Changamoto hizo ni: Ukataji miti kwa ajili ya
kuni, mkaa, mbao/ujenzi pamoja na uchomaji moto ovyo. Utafiti unaonesha kuwa takriban
Hekta 400,000 zinapotea kila mwaka kutokana na ukataji miti.
Changamoto nyingine inayotukabili ni kuwa na Idadi kubwa ya Mifugo ambayo
haiwiani na uwezo wa eneo la malisho hasa katika Mikoa ya Shinyanga, Rukwa Mwanza,
Morogoro n.k. Hali hiyo inasababisha Wafugaji kuvamia maeneo ya vyanzo vya maji pamoja
na maeneo ya hifadhi, na kuleta mmomonyoko wa udongo na hivyo kusababisha uharibifu
mkubwa wa mazingira. Uchafuzi wa Mazingira ya Makazi kumekuwepo na mazingira ya uchafu
katika makazi ya Watu na hasa maeneo ya Miji kutokana na kukosekana kwa namna nzuri
ya uondoshaji wa taka ngumu na laini.
Mheshimiwa Spika, Serikali
kwa kushirikana na Wananchi imeendelea na juhudi za kupambana na uharibifu wa mazingira
kwa kuchukua hatua mbalimbali. Hatua hizo ni pamoja na kuhimiza na kusimamia zoezi
la upandaji wa miti kila mwaka; kupanua mashamba ya miti ya Serikali kila mwaka, kusimamia
Sheria zinazozuia ukataji miti ovyo, kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaochoma
moto ovyo, kuweka Vituo vya Maliwato kwenye Vituo vya Mabasi na kwenye Barabara Kuu,
kutenga maeneo ya kukusanyia taka ngumu na Vimiminika Mijini, kuweka mazingira ya
Miji kuwa safi na kuhimiza uchimbaji na matumizi ya vyoo n.k. Napenda kuchukua fursa
hii kupongeza Mikoa na Halmashauri mbalimbali ambazo wamekuwa wakifanya juhudi kubwa
kuhimiza na kusimamia usafi katika maeneo yao. Nimekuwa nikishuhudia ubunifu mkubwa
katika suala hili la usafi wa Miji.
Nawaomba Viongozi
kwa kushirikiana na Wananchi kusimamia suala la kutunza Mazingira katika maeneo yao.
Tuzidi kuimarisha usafi wa mazingira, tusimamie zoezi la upandaji miti kuanzia kwenye
nyumba tunazoishi, Barabara, mashamba, Viwanja n.k. Tutunze vyanzo vya maji, tuzuie
uchomaji moto ovyo, tuwaelimishe Wafugaji kupunguza idadi ya mifugo ili iendane na
maeneo yao ya kulishia na tuchukue hatua zozote zinazoboresha mazingira ili tuwe na
maendeleo endelevu.
Mradi wa Uendelezaji na
Kuboresha Miji Nchini (Tanzania Strategic Cities Program (TSCP)
Mheshimiwa
Spika, Tarehe 18 Juni, 2013 nilipata fursa ya kuzindua mradi wa
kuboresha Miji Nchini katika hafla iliyofanyika Mjini Moshi. Mradi huu unatekelezwa
katika Miji 18 ya Tanzania Bara ikiwemo Miji ya Morogoro, Tabora, Moshi, Sumbawanga,
Shinyanga, Songea, Singida, Musoma, Iringa, Njombe, Lindi, Bukoba, Kibaha, Babati,
Geita, Korogwe, Mpanda na Bariadi. Mradi huo umetanguliwa na mradi mwingine wa
Kuboresha Miji Tanzania (Tanzania Strategic Cities Programme) ulioanza mwaka 2010.
Katika mradi huo kuna Halmashauri saba (7) za awali ambazo zinatekeleza Mradi huo.
Halmashauri hizo ni Arusha, Mwanza, Kigoma, Mbeya, Dodoma, Tanga na Mtwara Mikindani
pamoja na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA). Kwa hatua iliyofikiwa katika
utekelezaji wa Mradi huu umebadilisha sura na Mandhari ya Miji hiyo na kuifanya ivutie
kwa uwekezaji na kurahisisha utoaji wa huduma nyingine za Kijamii.
Mheshimiwa
Spika,
Napenda kutumia fursa hii kuzipongeza Halmashauri hizo
saba (7) pamoja na CDA kwa kufanya vizuri katika kutekeleza mradi huo na hivyo kuiwezesha
Benki ya Dunia kukubali kugharamia awamu nyingine ya Programu ya kuboresha Miji Nchini
kwenye Halmashauri za Miji mingine 18, ambayo nimeizindua hivi karibuni pale Moshi.
Benki ya Dunia pia imekubali kugharamia Mradi wa Kuboresha Jiji la Dar es Salaam (Dar
es Salaam Metropolitan Development Project-DMDC) ambao utaanza kutekelezwa wakati
wowote kuanzia sasa. Miradi hii mikubwa ya kuboresha Miji niliyoitaja itagharimu Dola
za Kimarekani Milioni 455 kutoka Benki ya Dunia. Fedha hii inategemewa kutumika katika
ujenzi wa jumla wa Miradi Midogo Midogo zaidi ya Kumi (10) itakayojumlisha barabara,
mifereji, Mifumo ya Uzoaji Taka, Taa za Barabara, maeneo ya Kuegesha Magari, Masoko,
Mipango Miji, Ukusanyaji Mapato ya Halmashauri, Uwajibika na Makazi holela. Ujenzi
wa barabara katika Jiji la Dar es Salaam unajumuisha pia Barabara za Juu (Fly Overs)
pale Ubungo. Sote tunakubaliana kwamba miradi hii ikikamilika, Miji hiyo itakuwa na
Mandhari nzuri kwa Wananchi na kuwa kivutio kikubwa kwa Wawekezaji kutokana na kuboreshwa
kwa madhari za kuweka mazingira ya usafi.
Mheshimiwa Spika, Nitumie
nafasi hii kuishukuru Benki ya Dunia kwa kukubali kugharamia Miradi hii. Ni dhahiri
tunafanya vizuri na ni wajibu wa kila mmoja wetu kusimamia Miradi hii itekelezwe vizuri
kwa ubora unaostahili. Ili kuhakikisha kwamba mafanikio yanapatikana katika miradi
hii, niwasisitize Wakurugenzi na Wakuu wa Idara wa Halmashauri kusimamia kwa karibu
utekelezaji wa miradi hiyo. Vilevile, Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakandarasi wawajibike
ipasavyo ili Mpango huu utekelezwe kwa wakati. Aidha, Halmashauri zote Nchini zijenge
tabia ya kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kutunza Barabara zinazojengwa ili
ziweze kudumu kwa muda mrefu na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa
Spika, Pamoja na mafanikio yanayoonekana wazi katika miradi hii,
changamoto nyingine kubwa tuliyonayo kwenye Mpango huu, wa kuboresha Miji ni kuona
Sehemu kubwa ya Miji yetu inaendelea kukua kiholela bila kuwepo kwa mipango makini
ya kuongoza ukuaji wa Miji hiyo. Napenda kutumia fursa hii kuziagiza Halmashauri zote
Nchini zisimamie kikamilifu upangaji Miji ili kuzuia ongezeko la ujenzi holela na
uharibifu Miji, hali inayotugharimu fedha nyingi katika kuipanga upya. Aidha,
Wananchi waelimishwe kuhusu umuhimu wa kuzingatia Sheria za uendelezaji Miji kwa mujibu
wa Sheria za Mipango Miji. Halmashauri zisimamie kikamilifu Sheria zinazokataza ujenzi
holela unaoharibu mandhari ya Miji yetu.
XI MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI
Mheshimiwa
Spika, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni Wadau muhimu wa maendeleo
ya Jamii na Taifa letu. Mashirika haya yamekuwa na mchango mkubwa hususan kwenye
nyanja za afya ikiwemo maradhi yanayotokana na UKIMWI, huduma za Maji, Elimu, Ushiriki
wa Jamii, Mazingira, Utawala Bora, Kilimo, Jinsia na Huduma kwa Yatima na Watoto wanaoishi
katika mazingira hatarishi. Aidha, Mashirika haya yamekuwa yakitoa ajira na fursa
za kupata uzoefu wa kujitolea kwa Watanzania. kwa Mfano katika mwaka 2012 zaidi ya
watu 60,700 waliajiriwa au kujitolea kwenye Mashirika haya.
Kwa
kuzingatia umuhimu huo, Serikali imekuwa ikijenga mazingira wezeshi ili yaendelee
kukua na kutoa mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya Nchi yetu. Mazingira hayo
ni pamoja kuyawezesha kutambulika kisheria kupitia usajili; pili, kuyalinda tatu,
kuwezesha ubia baina ya Serikali na Mashirika hayo na nne, kuyawezesha kujitawala
kupitia Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali.
Mheshimiwa
Spika, Kwa sasa, idadi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni kubwa
na imekuwa ikiongezeka kila mwaka huku mazingira ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali
kufanya kazi hapa Nchini yameendelea kuboreka. Kwa mwaka 2012/2013 pekee Jumla ya
Mashirika 443 yalisajiliwa na kufanya idadi ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali hapa
Nchini kufikia 5,734. Katika mazingira haya ikiwa kila Shirika lisilo la Kiserikali
litatekeleza ipasavyo malengo yake iliyojiwekea kwa mujibu wa Sheria, ni matumaini
ya Serikali kuwa hatua kubwa za maendeleo zitapatikana kwa haraka zaidi chini ya Mashirika
hayo.
Napenda kutumia fursa hii kuyataka Mashirika
yote kufanya shughuli zao kwa uwazi zaidi, kushirikiana na Serikali katika kuiletea
Jamii maendeleo. Pia Mashirika hayo yanakumbushwa kuwasilisha taarifa zao za mwaka
Serikalini kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 2002 kama ilivyorekebishwa
mwaka 2005. Vilevile, nawasihi kujiepusha na kujiiingiza katika masuala ya siasa na
uchochezi kwa raia. Kutofanya hivyo, kutayawezesha Mashirika haya kuaminika zaidi
katika Jamii na kuiwezesha Serikali kuainisha mchango wao katika maendeleo ya
Jamii yetu na Taifa kwa ujumla.
Kinachotakiwa ni kila Shirika
Lisilo la Kiserikali litimize wajibu wake kwa Wananchi ambao ndiyo walengwa bila ya
kujinufaisha yenyewe.
XII VYAMA VYA SIASA
Mheshimiwa Spika, Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa Na. 5 ya 1992 na Kanuni za Maadili
ya Vyama vya Siasa inaelekeza Wadau wote wa Demokrasia kutoa maoni yao kuhusiana na
marekebisho hayo kwa lengo la kukabiliana na changamoto za Kisiasa na Ki-utendaji
zilizopo na zitakazojitokeza katika masuala ya Siasa Nchini.
Mheshimiwa
Spika, Katika kuhakikisha kuwa amani inadumishwa Nchini. Ofisi
ya Msajili wa Vyama vya Siasa imewakutanisha Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi Nchini
na kuzungumza juu ya dhima ya Jeshi la Polisi na Vyama vya Siasa katika kukua kwa
Demokrasia na amani Nchini. Katika mazungumzo hayo Viongozi wa Vyama vya Siasa wamelaani
tabia ya baadhi ya Vyama vya Siasa kujihusisha katika kuvunja amani Nchini.
Mheshimiwa
Spika, Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio mengi ya
vurugu yanayohusishwa na Vyama vya Siasa. Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni zake
zinakataza Vyama kujihusisha na vurugu, kuigawa Nchi kwa udini, ukabila, rangi au
aina yoyote ya ubaguzi ambayo itasababisha kutoweka kwa amani ya Nchi. Vilevile, Sheria
hiyo imeweka bayana kuwa Chama kitakachobainika kufanya hayo, kitafutwa kwa mujibu
wa Sheria.
Mheshimiwa Spika, Napenda kuwakumbusha
Viongozi wenzangu hasa wa kisiasa kwamba, Demokrasia si kufuta Vyama wala kuvuruga
Nchi na kuwagawa Watanzania, bali ni kuwa na Sera nzuri zinazowaunganisha Watanzania
na kudumisha amani ya Nchi yetu. Kila Mtu pale alipo ana wajibu wa kulinda amani tuliyonayo
na kuhakikisha kuwa Sheria za Nchi zinazingatiwa kwa lengo la kulinda haki za Wananchi
wote. Nawaomba sana Wanasiasa na Viongozi wezangu tusijaribu kuweka rehani Nchi yetu
kwa kuhamasisha kwa njia moja au nyingine Wananchi wetu kuvuruga amani ya Nchi yetu.
Tuwafundishe Wananchi wetu kupendana kuvumiliana na kusaidiana.
XIII AMANI
NA UTULIVU NCHINI
Mheshimiwa Spika, Nimeongelea kuhusu Vyama
vya Siasa kutokana na hali halisi ya matukio yanayojitokeza Nchini. Hivi karibuni
pamekuwepo na matukio ya vurugu, fujo na uvunjifu wa amani katika maeneo mbalimbali
ya Nchi yetu. Katika kipindi cha mwaka mmoja tu uliopita vurugu zimetokea Arusha,
Mwanza, Mbeya, Mtwara, Morogoro, Singida na Iringa. Hofu ya migogoro ya kidini imetokea
Zanzibar, Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Geita. Baadhi ya matukio haya yamesababisha
Vifo na majeruhi ikiwemo, kujeruhiwa Askari na Wananchi, uharibifu wa miundombinu,
uharibifu wa mazingira na mali za Serikali na Watu binafsi.
Mheshimiwa
Spika, Matukio mfululizo ya fujo, vurugu pamoja na tukio la kulipua
mabomu Kanisani na hivi karibuni katika Mkutano wa hadhara huko katika Kata ya Soweto
kule Arusha na katika Mkutano wa Kampeni ya Chama cha Chadema katika Uwanja wa Soweto
Arusha yamesababisha hofu kubwa kwa Wananchi na hisia ya uwepo wa tishio la kuendelea
kwa vitendo vinavyoashiria ugaidi katika Nchi yetu. Matukio ya aina hii yakiachwa
yaendelee, uchumi wa Nchi yetu utadorora kutokana na ushiriki hafifu kwenye shughuli
za maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Vilevile, ziko
dalili ya kuwepo kwa vikundi vya Watu wachache wasioitakia mema Nchi yetu. Vikundi
hivi vinataka kupandikiza chuki za kisiasa na kidini miongoni mwa Watanzania na kuleta
mapigano na mauaji miongoni mwao. Sina shaka kuwa fujo, vurugu, vitendo vya uvunjifu
wa amani ikiwemo mashambulio ya Mabomu Arusha na vurugu za Mtwara ni sehemu ya mikakati
hiyo mibovu. Nataka niwahakikishie Watanzania kuwa Serikali haitavumilia hata kidogo
kuendelea kupandwa mbegu za chuki na za kidini na kisiasa miongoni mwa Watanzania.
Serikali itachukua hatua kali bila huruma kuzimaliza njama hizi mbaya dhidi ya Taifa
letu. Vilevile, hatua kali zitachukuliwa kwa Mtu yeyote atakayebainika kuhusika bila
kujali hadhi na nafasi yake katika Jamii.
Mheshimiwa Spika, Nitumie nafasi hii tena kuwasihi Viongozi wa Serikali, Kisiasa, Kidini
na Wananchi wote kwa ujumla, kila mmoja kwa nafasi yake kuwajibika ili kuhakikisha
kuwa Nchi yetu inaendelea kuwa Kisiwa cha Amani na Utulivu. Watanzania wote tushirikiane
na Vyombo vya Dola katika kubaini wahalifu hao. Tuendelee na mshikamano wa kukataa
vitendo vya uvunjifu wa Amani katika Nchi yetu. Kila mwenye taarifa za kuwezesha
kukamatwa kwa Watu wanaohatarisha amani ya Nchi yetu atoe taarifa kwa Jeshi letu la
Polisi na taarifa hizo zitafanyiwa kazi kwa umakini mkubwa na kwa maslahi ya Taifa
letu.
XIV HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Changamoto
kubwa iliyoko mbele yetu baada ya kuwepo hapa Bungeni kwa takriban Siku 78 ni kusimamia
utekelezaji wa Bajeti ya Serikali tuliyoipitisha. Sisi kama Wabunge tuondoke hapa
kwa lengo moja la kushirikiana na Wananchi kusukuma maendeleo na Bajeti tuliyoipitisha
ikiwa ndiyo kichocheo kikuu. Nchi yetu bado ni nzuri na ina amani. Wananchi wetu bado
ni Watu wazuri, wastaarabu, wavumilivu na wapenda amani. Wananchi wanaelewa na ni
watiifu. Twendeni tukasisitize umuhimu wa kuishi kwa amani, upendo na mshikamano.
Tukiwasimamia vizuri na kuwaongoza katika matumizi ya rasilimali zilizopo, Nchi yetu
itasonga mbele kimaendeleo na maisha bora kwa Wananchi wetu yatapatikana.
XV SHUKRANI
Mheshimiwa
Spika, Napenda nimalizie kwa kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha
Mkutano huu. Nikushukuru kwa namna ya pekee wewe mwenyewe Mheshimiwa Spika na Naibu
Spika kwa kutuongoza vizuri kulingana na Kanuni za Bunge. Aidha, niwashukuru Wenyeviti
wa Bunge, Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama, Mbunge wa Peramiho, Mheshimiwa Mussa
Zungu Azzan, Mbunge wa Ilala na Mheshimiwa Muhammed Seif Khatib Mbunge wa Uzini kwa
kuongoza vizuri baadhi ya Vikao vya Bunge wakati wa Mkutano huu. Ninawashukuru tena
Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu ya dhati na yenye mantiki kwa ajili ya
Maendeleo ya Nchi yetu. Niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Watumishi
na Wataalam wote wa Serikali waliosaidia kujibu Maswali na Hoja mbalimbali za Waheshimiwa
Wabunge zilizojitokeza hapa wakati wa Mkutano huu. Vilevile, nawashukuru Waandishi
wa Vyombo vya Habari kwa kuwapatia Wananchi habari kuhusu Majadiliano yaliyokuwa yanaendelea
hapa Bungeni. Wote kwa ujumla wenu nawashukuru sana.
Kipekee
napenda kuwashukuru Madereva wote ambao wamekuwa makini katika kazi ya kuwaendesha
Viongozi wote wakiwemo Waheshimiwa Wabunge na Wataalam kutoka sehemu mbalimbali Nchini
na kuwawezesha kufika hapa Dodoma kuhudhuria Mkutano huu wa Kumi na Moja. Vilevile,
nawashukuru Wananchi wa Mkoa wa Dodoma, Wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Dkt.
Rehema Nchimbi kwa ukarimu wao kwa muda wote tuliokaa hapa Dodoma. Navishukuru pia
Vyombo vya Ulinzi na Usalama ambavyo vimehakikisha muda wote tumekaa kwa Amani na
kwa Utulivu mkubwa. Mwisho namshukuru Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashilillah na Watumishi
wote wa Ofisi ya Bunge kwa huduma nzuri zilizowezesha kukamilisha shughuli zilizopangwa
katika Mkutano huu bila matatizo.
Mheshimiwa Spika, Nitumie
fursa hii kuwaombea safari njema mnaporudi katika maeneo yenu ya kazi. Lakini pia
niwaombee kheri na Baraka tele Waislamu wote ambao katika siku chache zijazo watashiriki
katika Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Kila atakayeamua kufanya Ibada hiyo aifanye
kikamilifu na kama Kitabu cha Quran Tukufu kinavyoelekeza.
Mheshimiwa
Spika, Baada ya maelezo hayo, napenda kutoa hoja kwamba, Bunge
lako Tukufu sasa liahirishwe hadi tarehe 27 Agosti, 2013 siku ya Jumanne, Saa 3:00
Asubuhi litakapokutana katika Mkutano wa 12 kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.