Kongamano la Kimataifa kufanyika Benin, kama kumbu kumbu ya Mwaka mmoja tangu Africae
Munus ilipochapishwa
Baraza la Kipapa la Utamaduni kwa kushirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Benin
pamoja na Taasisi ya Elimu Katoliki Ufaransa, kwa pamoja wameandaa Kongamano la Kimataifa,
kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka mmoja, tangu Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita, alipozindua Matunda ya Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu
Katoliki Afrika, huko nchini Benin, kunako Mwezi Novemba 2011. Viongozi mbali mbali
wa Kanisa kutoka Benin na Vatican wanatarajiwa kushiriki kuanzia tarehe 21 hadi tarehe
25 Januari 2013.
Kongamano hili la Kimataifa linaoongozwa na kauli mbiu "Haki,
utamaduni na Upendo". Wajumbe watapata fursa ya kusikiliza Falsafa inayofumbatwa
katika Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Dhamana ya
Afrika. Watajadili kwa kina na mapana kuhusu: haki na kipindi cha mpito kuelekea demokrasia;
haki na utamaduni; vita vya wenyewe kwa wenyewe na mauaji ya kimbari; haki na upendo;
mchango wa dini mbali mbali katika kudumisha fadhila hii.
Hapo tarehe 25 Januari
2013, wajumbe watahitimisha kwa kutoa muhtasari ya yale yatakayojiri kwenye kongamano
ili yaweze kufanyiwa kazi katika mchakato wa kudumisha haki, amani na upatanisho.